WEZESHA WANAWAKE

WEZESHA WANAWAKE

Thursday, May 3, 2012

LEO NI SIKU YA UHURU WA HABARI DUNIANI...


Leo tarehe 3 Mei ni siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo huadhimishwa ulimwenguni kote. Siku hii ili ilitangazwa rasmi na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuamsha Ufahamu wa Umuhimu wa Uhuru wa Habari na kuzikumbusha Serikali Wajibu wao katika Kuheshimu na Kusimamia Uhuru wa Kujieleza. Msingi wa Wajibu huu unapatikana katika katika Kifungu cha 19 cha Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lililotolewa Ufaransa mwaka 1948 baada ya Matukio ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Pamoja na Siku hii kuwa na msingi wa kimataifa, Waandishi wa Magazeti  wa Afrika waliokutana Windhoek, Namibia katika semina iliyoandaliwa na UNESCO walitoa Tamko la Windhoek la Misingi ya Uhuru wa Habari mwaka 1991.

Hivyo siku hii ya Uhuru wa Vyombo vya habari inatokana na misingi mbalimbali madhubuti inayolenga kuhakikisha Heshima, Umuhimu na ulinzi wa misingi ya Uhuru wa habari.
Ofisi za UNESCO Makao Makuu

UNESCO huwa inaadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari kwa kutoa Tunzo ya Guillermo Cano kwa mtu binafsi, kampuni au taasisi iliyotoa mchango mkubwa kulinda na kutetea uhuru wa habari popote duniani hasa pale utetezi huu unapotokea kwenye mazingira hatarishi. Tunzo hii ilianza kutolewa mwaka 1997 ambapo kamati ya nguli 14 weledi katika tasnia ya Habari wanoachaguliwa na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO na kutumikia kipindi cha miaka mitatu, hupendekeza jina la atakayepokea Tunzo katika mwaka husika. Jina hilo hutokana na mapendekezo kutoka Taasisi zisizokuwa za kiserikali za kikanda na kimataifa zinazojishughulisha na Uhuru wa Habari na nchi wanachama wa UNESCO.



Kamati iliyohusika katika uteuzi wa jina la mpokea Tunzo wa Mwaka huu inaongozwa na Diane Senghor kutoka Senegal ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa wa Taasisi ya Kuendeleza Utamaduni wa Kidemokrasia na Majadiliano. Wengine katika kamati hiyo ni Alexandra Föderl-Schmid (Austria), Bulbul Monjurul Ahsan (Bangladesh), Miklos Haraszti(Hungary), Ognian Zlatev (Bulgaria), Daniel Santoro (Argentina), Steven Gan (Malaysia), Fatuma Noor (Kenya), Rossana Fuentes-Berain (Mexico), Rana Sabbagh, (Jordan), Gamal Eid (Misri), Florence Aubenas (Ufaransa).
Tunzo hiyo imepewa jina la Guillemo Cano Isaza ambaye alikuwa Mwandishi wa habari aliyeuwawa mbele ya ofisi za gazeti analoliandikia la El Espectador mwaka 1986 baada ya kuanzisha kampeni ya ushawishi wa wauza madawa ya kulevya katika siasa nchini  Colombia.

Guillermo Cano, Mwandishi wa Habari aliyeuwawa mbele ya Ofisi ya Gazeti lake mwaka 1986
Mwaka huu, 2012, Siku hii ya Uhuru wa Vyombo vya Habari inaadhimishwa Tunisia ambapo Mkurugenzi wa UNESCO, Irine Bokova amemtangaza, Mwanaharakati na Mwandishi wa Habari wa Azberjani, bwana  Eynulla Fatullayev (35) kuwa mshindi wa Tunzo ya Guillemo Cani.
Eynulla Fatullayev (35) Mshindi wa Tunzo ya Guillemo Cani mwaka 2012
Eynulla Fatullayev alikuwa Mhariri Mkuu na Muasisi wa Gazeti la wiki la “Realny Azerbaijan” lililokuwa likiandikwa katika lugha ya Kirusi na gazeti la kila siku la “Gundalik Azarbaycan” lililokuwa likiandikwa katika lugha ya Kiazabejaini.
Azerbejaini ni nchi inayopatikana katika ya Bara la Asia na Ulaya ikipakana na bahari ya Caspian, Urusi, Georgia, Armenia na Urusi. Mara nyingi nchi hii imekuwa ikihesabiwa kama nchi ya Ulaya kutokana na kuwa Mwanachama wa  Baraza la Ulaya Tangu mwaka 2001 ingawaje kijografia huwa inahesabiwa kama sehemu ya Asia Magharibi.
Katika taaluma yake Eynulla Fatullayev amekuwa akipigania, kutetea na kusimamia Uhuru wa Habari na Uhuru wa Kujieleza. Harakati hizi zilisababishwa kutiwa hatiani na kufungwa mwaka 2007 mpaka alipoachiwa kwa msamaha wa Raisi siku ya kuadhimisha sikukuu ya Jamhuri ya Azerbajaini  tarehe 26 Mei mwaka 2011. Mara tu baada ya kuachiwa huru alianzisha taasisi isiyokuwa ya serikali “Public Union for Human Rights”. Tunzo hii inakwenda kwake kwa kutambua mchango wake kwa kuzingatia misingi na vigezo vilivyowekwa katika kumpata mshindi.
Mpaka sasa tunzo hii imeshakwenda kwa wanahabari 16 wakiwemo wawili kutoka katika bara la Afrika. Waandishi na wanaharakati wengine waliowahi kupata tunzo hii tangu ilipoanzishwa ni pamoja na:
      1.      Gao Yu (China, 1997)
2.      Christina Anyanwu (Nigeria, 1998)
3.       Jesus Blancornelas (Mexico, 1999)
4.      Nizar Nayyouf (Syria, 2000)
5.      U Win Tin (Myanmar, 2001)
6.       Geoffrey Nyarota (Zimbabwe, 2002)
7.       Amira Hass (Israel, 2003)
8.       Raúl Rivero (Cuba, 2004)
9.      Cheng Yizhong, (China, 2005)
10.  May Chidiac (Lebanon, 2006)
11.  Anna Politkovskaya (Russian Federation, 2007)
12.  Lydia Cacho (Mexico, 2008)
13.  Lasantha Wickrematunge (Sri Lanka, 2009)
14.  Mónica González Mujica (Chile, 2010)
15.  Ahmad Zeidabadi (Iran, 2011)
Huku ndiko ilikotoka tunzo ya Guillemo Cano ambayo hutolewa kila mwaka katika maadhimisho ya Siku ya Vyombo vya habari duniani.

Hongera wanahabari wote Duniani...
Hongera wanahabari wote Tanzania...
(Habari kwa hisani ya UNESCO na Wikipedia)

No comments:

Post a Comment