WEZESHA WANAWAKE

WEZESHA WANAWAKE

Saturday, April 28, 2012

Homa ya Manchester Derby Jumatatu 30/4/2012

Ikiwa imebaki siku moja kabla miamba miwili ya soka ya Manchester haijakutana Jumatatu tarehe 30 April 2012, joto na hamasa za wachezaji, mashabiki, watazamaji na wadau wote zinazidi kupanda.
Manchester Derby ni jina linalotambulisha mchezo unaozikutanisha timu mbili zinazotoka Manchester yaani Manchester City wanaotoka mashariki mwa Manchester wenye maskani yao Etihad Stadium na Manchester United wanaotoka Trafford wenye maskani yao Old Trafford
Manchester City FC

Manchester United FC
Timu hizi zimekuwa na rekodi ya mahudhurio makubwa zaidi ya watazamaji katika mechi zao za nyumbani. Tiketi kwa ajili ya kuingia uwanjani Etihad Stadium tarehe 30 Aprli 2012 zilikuwa zimekwisha (zimeuzwa zote) zaidi ya wiki mbili kabla ya pambano.
Mechi ya mwisho kati ya timu hizi mbili ambayo ni ya 162 baina yao, ilikuwa kwenye mzunguko wa tatu wa Kombe la FA, Januari 8, 2012 Etihad Stadium ambapo Manchester United iliondoka na ushindi wa magoli 3 – 2. Mechi inayofuata itakuwa Jumatatu tarehe 30 April 2012 kwenye uwanja huo huo wa Etihad.
UMUHIMU WA MECHI HII KWA TIMU ZOTE
Katika msimamo wa ligi hivi sasa, timu ya Manchester United iko mbele ya Manchester City kwa pointi tatu (3) huku timu zote zikiwa zimecheza michezo 35. Hivyo basi kuna uwezekano wa Manchester City kuongoza ligi endapo itaifunga Manchester United Jumatatu.
 Matokeo ya mechi mbalimbali baada ya tarehe 8 Aprili 2012 yamegeuza muelekeo na hamasa ya kunyakua ubingwa kwa timu hizi mbili. Baada ya Manchester United kuifunga Queens Park Rangers (QPR) magoli 2 – 0 na Manchester City kufungwa goli 1 – 0 na vijana wa Arsene Wenger, Arsenal, pale Etihad tarehe 8 Aprili, 2012 ilionekana wazi kuwa mbio za kunyakua ubingwa wa EPL zilikuwa zimefikia ukingoni. Tofauti ya pointi nane kati ya timu hizi mbili zilizokuwa zikifukuzana kwenye uongozi wa ligi iliifanya timu ya Manchester United kuwa na nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa na kuacha nafasi finyu kwa wapinzani wao Manchester City kuchukua ubingwa huo.
Upepo ulianza kugeuka taratibu pale Manchester United walipokutana na Wigan Athletic tarehe 11 April 2012 kwenye uwanja wa DW stadium na kupata kipigo cha goli 1 – 0 huku wapinzani wao Manchester City wakiwashushia kipigo cha magoli 4 – 0 West Brom siku hiyo hiyo. Ushindi huu wa Manchester City ulianza kupunguza tofauti ya pointi baina yake na Manchester United kutoka nane hadi tano; hali kadhalika kujiongezea akiba ya magoli ya kufunga ambayo pia imekuwa silaha ya timu hii pale inapotokea kufunga kwa pointi na mshindani wake.
Yule Bundi mweusi aliendelea kukaa kwenye paa ya nyumba ya Manchester United pale walipokutana Timu ya Everton katika uwanja wa Old Traford Jumapili tarehe 22 Aprili 2012 na kulazimishwa sare ya magoli 4 – 4 huku wapinzani wao Manchester City wakiifunga the Wolves mabao 2 – 0 na kuishusha daraja. Matokeo haya ya Jumapili yalizidi kutia Nuru kwenye jitihada za Manchester City kunyakua Ubingwa wa EPL huku yakipeleka wasiwasi mkubwa kwa wapinzani wao wa Old traford kwani tofauti ya Pointi sasa ilikuwa ni Pointi 3
Hakuna shaka kuwa matokeo na muendelezo huo katika ligi hasa kwa vigogo hivi viwili vya Manchester unaufanya mpambano wa Jumatatu 30, Aprili 2012 kuwa mpambano muhimu sana kwa kila timu na kuongeza hamasa kwa wadau kushuhudia pambano hilo.
Kati ya mwaka 1992 mpaka 2011 kumekua na mashindano 19 ya ubingwa wa ligi ya premier ambapo Manchester United imefanikiwa kuchukua ubingwa huo mara 12. Kwa takwimu hizo ni Manchester United ambayo imechukua ubingwa mara nyingi zaidi kuliko klabu nyingine yoyote, ubingwa wa mwisho ukiwa ule aliouchuku msimu wa 2010/11. Mashabiki na wapenzi wa Manchester united hawangependa kupoteza historia na muendelezo huo wa ubingwa.
Kwa misimu miwili mfululizo, Manchester City imewekeza katika kununua wachezaji mahiri katika harakati zake za kujiimarisha na kunyakua ubingwa ambao hawajawahi kuutwaa na hivyo ni mategemeo ya mashabiki wake kulinyakua kombe hilo mwaka huu. Manchester City wasingependa kuona jitihada hizi zikienda bure hasa katika kipindi hiki ambacho matumaini ya ushindi yamerudi tena baada ya kupotea pale April 8 2012. Mashabilki, wapenzi na wadau wote wangependa kuona kwa mara ya kwanza ubingwa unabaki Etihad. Mchezaji mahiri na kocha wa Zamani wa Manchester City, Kevin Keagan anaamini kuwa ushindi wa katika mechi yake na Manchester United Jumatatu, itaihakikishia timu hiyo Ubingwa msimu huu na kulibakiza kombe Etihad.
Kevin Keagan, Kocha wa Zamani wa Manchester City
Makocha wa timu zote mbili wanajua umuhimu wa mechi hii huku Kocha wa Manchester United Sir Alex Fergusson akisema kuwa mechi hii ndio muhimu zaidi katika miaka yake yote 26 katika uongozi wa soka ....“Ni mchezo muhimu ambao utaamua bingwa , tuna nafasi nzuri zaidi kuliko Man City. Wenyewe wanahitajika kushinda, sisi tunaweza kutoka sare au kushinda. Tutajitahidi kushinda”
Kocha wa Manchester United, Sir Alex Fergusson
Manchester City haijafanikiwa kushinda katika mechi zake tatu za kombe la Premier zilizochezwa uwanja wa nyumbani Etihad lakini itakuwa ikijiamini kutokana na ushindi wake wa magoli 6 – 1 dhidi ya Manchester United Mwezi October 2011.
Kocha wa Manchester City Roberto Mancini anaona kuwa Manchester United bado wana nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa wa Premier Ligi pamoja na ukweli kwamba kuna tofauti ya pointi tatu tu baina ya timu hizo mbili. Mancini alisema kuwa “Ni muhimu kushinda katika mchezo huu, kiwango si muhimu sana , tumecheza vizuri katika msimu mzima lakini cha muhimu kwa sasa ni Kushinda”
Kocha wa Manchester City, Roberto Mancini
Baada ya hekaheka za Champions league zilizohusisha miamba ya Hispania Barcelona na Real Madrid; Macho na masikio ya wapenzi wengi wa soka yako Etihad Jumatatu tarehe 30 Aprili 2012

No comments:

Post a Comment