WEZESHA WANAWAKE

WEZESHA WANAWAKE

Monday, April 23, 2012


HATIMAYE BINGU WA MUTHARIKA AZIKWA “TAJ MAHAL”
Marehemu Bingu wa Mutharika (1934 - 2012)

Bingu wa Mutharika (78) aliyefariki tarehe 5 Aprili 2012 kwa ugonjwa wa Moyo, Hatimaye amezikwa “Maphumulo wa Bata,” jina la lugha ya kichewa linalomaanisha Pumziko la Amani, Sehemu ambayo imekuwa pia ikiitwa Taj Mahal. “Maphumulo wa Bata,” imejengwa kwenye Shamba binafsi la marehemu Bingu wa Mutharika huko Ndata

Maphumulo wa Bata ambapo pia hujulikana kama Taj Mahal

Pameitwa Taj Mahal kulinganisha na Taj Mahal iliyoko Agra India iliyojengwa na Mtawala Shah Jahan kwa kumbukumbu na Mazishi ya Mke wake wa tatu Muntaz Mahal ambako hatimaye Shah Jahn alizikwa pia. Taj Mahal ya India inatokana na kazi ya Usanifu wa Ujenzi wa Mughal, yenye muundo wa ujenzi unaojumuisha utaalamu wa Ki-persia, Kihindi, kituruki na ustaarabu wa kiislamu.
Taj Mahal Halisi iliyoko Agra, India iliyojengwa na Mtawala Shah Jahan

“Maphumulo wa Bata,” umepewa jina la Taj Mahal kutokana na ukubwa wake na ueledi uliotumika kati Usanifu wa ujenzi wake na gharama kubwa iliyotumika katika Ujenzi wake. “Maphumulo wa Bata,” ilijengwa na Marehemu Bingu wa Mutharika kwa ajili ya Maziko ya mke wake Ethel Bingu wa Mutharika aliye fariki mwaka 2007. Kama ilivyokuwa kwa Mtawala Shah Jahan, Bingu wa Mutharika naye amepumzishwa “Maphumulo wa Bata,” au Taj Mahal kama inavyojulikana huko Malawi. Bingu wa Mutharika alitaka eneo hilo kuwa Mnara wa taifa ambao utatembelewa na wamalawi kama sehemu ya Makumbusho ya Taifa. Ni katika Shamba hilo pia ambako Bingu wa Mutharika alijenga Kasri kubwa yaKifahari ambayo ililalamikiwa sana na wananchi wa Malawi wakati wa Ujenzi wake wakihusisha ujenzi huo na ubadhirifu mkubwa wa Fedha za Malawi mara baada ya Kuchaguliwa kuwa Raisi mwaka 2004
Kasri ya Bingu wa Mutharika iliyojengwa kwenye Shamba lake Ndata
Bingu wa Mutharika, Mwanasiasa na Mchumi alichaguliwa kuwa raisi wa tatu wa Malawi kwa mara ya kwanza Mwezi Mei, 2004 na aliendelea kuwa Raisi mpaka alipofariki. Bingu wa Mutharika alikuwa pia Raisi wa Democratic Progressive Party ambayo ndio ina wabunge wengi zaidi bungeni baada ya Uchaguzi mkuu wa Mwaka 2009.
Mazishi ya Bingu wa Mutharika yamehudhuriwa na watu mbalimbali mashuhuri wakiwemo Maraisi kadha wa Afrika kama Robert Mugabe wa Zimbawe, Mwai Kibaki wa Kenya, Armando Guebuza wa Msumbiji, Hipikefunye Pohamba wa Namibia na Jakaya Kikwete wa Tanzania ambao pia walihudhuria ibada ya Mazishi mjini Blantyre, Malawi.
Gharama za mazishi ni kiasi cha kwacha milioni 242 ambazo ni sawa na Dola za Marekani Milioni Moja na nusu (US $ 1.5m)
Kwa heri Bingu wa Mutharika, Kwa heri Raisi wa Tatu wa Malawi


No comments:

Post a Comment