WEZESHA WANAWAKE

WEZESHA WANAWAKE

Sunday, May 6, 2012

Mabao 5 ya Simba yahitimisha Ligi Leo...


Wachezaji na viongozi wa Simba wakishangilia Kombe baada ya Kuifunga Yanga 5 - 0

Ubao wa Matokeo dakika ya 84 ambao uliendelea kusomeka hivyo mpaka mwisho wa Mchezo

Filimbi ya Mwisho ilipopigwa katika Uwanja wa Taifa kuashiria mwisho wa mchezo kati ya Simba na Yanga ambao umekuwa ukisubiriwa kwa Hamu, Ubao wa Matokeo pale uwanjani ulisomeka Simba 5 - Yanga 0. Huu ni kati ya Ushindi mkubwa kwa magoli mengi baina ya timu hizi mbili ukiacha ule ushindi wa Simba dhidi ya Yanga mwaka 1977 ambapo timu ya Yanga ilifungwa mabao 6 - 0.
Kikosi Cha Simba kikiwa tayari kwa mtanange na watani wa jadi Yanga
Kikosi cha Yanga kikiwa tayari kuumana na watani wake wa Jadi Simba

Kama ilivyo kawaida katika soka la Tanzania, Mechi ya Simba na Yanga huvuta hisia za mashabiki wengi wa Soka hapa nchini kwani timu hizi zimekuwa na Historia kubwa ya Ushindani huku ukiwa na Mashabiki wengi.
Mpambano kati ya timu hizi mbili umekuja wakati Simba ikiwa imeshanyakua ubingwa kutokana na wingi wa Pointi ambazo zisingeweza kufikiwa na timu nyingine yoyote. Kutokana na matokeo ya timu ya Yanga kutokuwa mazuri ligi ilipokuwa ikielekea ukingoni, Yanga ilipoteza matumaini ya kuchukua ubingwa wala kuwa mshindi wa pili. Aidha mgogoro uliokuwa ukifuka moshi ndani ya klabu ya Yanga haukuwa ishara njema kwa matokeo ya michezo mbalimbali iliyokuwa ikiwakabili. Katika wiki za karibuni tumeshudia wazee wa Yanga wakitangaza kukabidhiwa timu Huku mwenyekiti akipinga uhalali wa maelezo hayo.

Pamoja na yote yaliyokuwa yakiendelea katika vilabu hivi bado umuhimu, kukamiana na hamasa ya mechi baina ya watani hawa wa jadi uliendelea kuimarika na kuwepo.

Alipohojiwa jana Jumamosi kabla ya mechi, Kocha wa Simba Cirkovic Milovan alisema kuwa huu ni mpambano muhimu zaidi katika maisha yake ya Soka pale Msimbazi. Alisema kuwa pamoja na ukweli kwamba Timu ya Simba ilikuwa imeshanyakua ubingwa, ushindi katika mechi yake na timu ya Yanga ulikuwa ni wa Muhimu sana.  

Uwanja wa Taifa ulifurika mashabiki wa timu zote mbili wakijinadi kwa jezi zenye rangi za vilabu vyao.
Mashabiki wa Simba

Mashabiki wa Yanga

Mpira ulianza kwa mashamu shamu huku nyimbo, mbinja, vifijo, sauti za mavuvuzela zikitawala uwanja wa Taifa. Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, Timu ya Simba ilikuwa ikiongoza kwa Goli moja ambalo lilifungwa na Emmanuel Okwi.
Emmanuel Okwi akishangilia Goli lake la kwanza

Kipindi cha pili kilipoanza wachezaji wa Simba walionekana wakiwa na Ari kubwa ya kuimarisha ushindi wao ambapo tulishuhudia magoli manne yaliyofungwa na Felix Sunzu (Penati dakika ya 55), Emmanuel Okwi (Dakika ya 63), Juma Kaseja(Penati) na Patrick Mafisango (Penati)

Kwa magoli yaliyofungwa kipindi cha Pili na lile la kipindi cha kwanza mpaka kipenga cha mwisho kinapulizwa, timu ya Simba ilikuwa imeandika magoli 5 - 0.
Huu ni ushindi ulioweka rekodi katika ligi pale zinapokutana siku hizi mbili za Simba na Yanga katika miongo miwili.

Kama ilivyokuwa kwa Maurinho baada ya Real Kuchukua ubingwa,Cirkovic Milovan alijikuta hewani kutokana na furaha ya wachezaji na viongozi kutwaa ubingwa na kuifunga Yanga 5 - 0

Mgeni Rasmi katika Mchezo huu alikuwa Waziri Mteule wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk Fenela Mkangara

Kapteni, Juma Kaseja akipokea Kombe toka kwa Mgeni Rasmi, Waziri Mteule wa Habari, ijana, Utamaduni na Michezo Dr. Fenela Mukangara

HONGERA SIMBA SPORTS CLUB!

No comments:

Post a Comment